Chereads / Tafadhali, Nipende(Please, Love me) / Chapter 231 - USINIACHE

Chapter 231 - USINIACHE

Usiku wa siku iliyopita baada ya chakula cha jioni, Li alikusudia kurudi nyumbani kwa Ed akiamini Beruya angeendelea vyema katika uangalizi wa mama yake. Akaelekea chumbani kwa mama yake ambaye mara nyingi unaendelea kulala mapema. Akagonga mlango, sauti ya mama ikamuitikia kumpa ruhusa aingie.

"Mwanangu" akainuka na kuketi kitandani akimtazama mwanae ambaye aliingia na kusimama pembeni karibu na mlango

"Njoo ukae hapa sasa utabaki umesimama" akamwambia huku akimuonesha sehemu ya kitanda aweze kuketi

Li akasogea na kuketi kisha akamwambia, "mama nimekuja kukuaga naru__"kabla hajaendelea mama akamshika mkono

"Aishhhhh mbona haraka hivyo mwanangu" akalalamika

"Mama, kule kazini nina mambo yananisubiri na pia nataka nikamwangalie Allan anaendeleaje" Li akajitetea huku akichukua mkono wa mama yake na kuweka kati ya viganja vyake

"Nimemwambia Samir asimamie, Allan sina shaka nae kabisa. Baki hapa kwa siku mbili umsaidie huyo binti" mama akamwambia kwa upole

Li akatabasamu kisha akambonyeza mkono "mama Beruya yuko salama na wewe, kaka Ed aliamini hivyo ndio maana hakuniambia nimpeleke kule Diamond. Ila nakuahidi nitakuja kila jioni kumuona. Najua anatakiwa kuanza tena kuchora, nitakuja mara zote kuhakikisha yuko salama. Derrick atakuja na meneja wake pia watakuwa nae. Please ma!"

Mama yake akamwangalia kisha akatabasamu, "Haya mwanangu, lakini hakikisha unaongea nae kwanza kabla ya kuondoka"

"Sawa mama, naona unavyomfurahia" akamtania huku akiinuka kuondoka

"Hahahaha ni mimi au wewe eeeh!" Mama nae akarudisha utani ule

Li akatikisa kichwa kukataa huku akielekea mlangoni lakini neno lililofuata likamfanya asimame

"Furaha yangu ni kuona unaniletea mkwe!" Mama akajinyoosha kulala

"Mama tafadhali usi__" Li akajaribu kuongea lakini mama akamuwahi

"Nisiseme eeeh! Kuna wakati vitu vizuri vinakuja mlangoni kwako unakataa kuviona. Usisahau kwenda kumuaga" mama alipomaliza, akajifunika shuka hadi usoni

Li akashusha pumzi na kugeuka kuelekea mlangoni, akatoka. Moyoni akapuuzia kile alichoambiwa na mama yake kwa kuwa hakuona kama ni kitu kinachowezekana.

Akaelekea chumbani kwa Beruya akagonga mlango mara ya kwanza kisha akatulia kusikia kama kuna mtu angekuja

Alipofanya hivyo mara ya tatu akaamua kufungua taratibu, Beruya alikuwa amelala. Aliposogea akagundua Beruya alikuwa akiweweseka usingizini, alijikunyata huku mwili wake ulitetemeka kama mtu aliyepatwa na baridi. Li aliposogea alichoshangaa ni kuona kwenye paji la uso wake likiwa na matone ya jasho huku midomo yake ikimung'unya maneno yasiyoeleweka. Michirizi ya machozi ililowanisha sehemu ya mto wake....

Akamgusa begani huku akimuita taratibu "Beruya" lakini badala ya kufumbua macho alizidi kujikunyata huku akitetemeka. Li akainama aweze kusikia maneno ambayo aliyasema, akainama hadi usawa wa uso wake. Alichokisikia kilimshtua Li

"Nn..nnisaidie....tta tafadhali....usiniache"

Li akashikwa na huzuni kwa namna ambavyo alimuona Beruya akiweweseka.

"Sijui nini kimemsibu huko ndotoni" akaamua kumshika ili apate kumgeuza.

"Beruya" akamuita ili kumtoa kwenye jinamizi lililompata ndotoni, akamgeuza na ghafla Beruya akashtuka na kuinuka kama mtu aliyetaka kukimbia macho yake yakiwa bado usingizini. Li akamshika kwenye mabega ili kumrudisha katika uhalisia lakini Beruya akamkumbatia huku akiendelea kusema "tafadhali nisaidie"

Li ghafla akawa kama barafu kwa namna alivyoshtushwa na kitendo kile. Mikono ya Beruya iliyopita shingoni kwake ilipozidi kumkamata akahisi kuitafuta hewa. Akapitisha mkono mmoja usawa wa tumbo na mwingine ukabaki mgongoni mwake akimpapasa taratibu ili kumpa uhakika

"Uko salama Beruya. Usiwe na shaka. Niko hapa" aliendelea kumwambia taratibu huku akiyashangaa mwenyewe maneno yake

"Usiogope niko hapa. Uko salama" baada ya muda mikono ya Beruya ikalegea shingoni mwake na kwikwi iliyoambatana na machozi ikaanza kupungua. Sasa Beruya alirudi kulala mikononi mwa Li.

Alipoona hivyo Li akaamua kumrudisha alale vyema pale kitandani lakini Beruya alirudia kumkamata vyema shingoni huku akinong'ona "tafadhali usiniache"

Li akashusha pumzi!