Baada kukata simu Aretha ambaye aliketi pembeni ya Ed kwenye kochi la mgahawa uliokuwa ndani ya uwanja wa ndege wa Kuala Lumpur, alimtazama kwa furaha,
"Asante Rian" akasema Aretha huku akipitisha mkono wake kwenye kwapa la Ed kwa furaha
"Hahahah umetusikiaje wakati natumia 'pods' Retha" akauliza kwa utani huku akimfinya kwenye shavu
"Hahah hapana, majibu yako nimeyasikia" Aretha akamjibu huku akiegamia begani kwa Ed..
Edrian alifurahi kumuona Aretha mwenye furaha. Mle ndani kila mtu alikuwa na mambo yake na hakuna aliyewatazama japokuwa mara kadhaa Aretha aliwaona watu waliowashangaa kuona wakizungumza lugha tofauti na kiingereza.
Walipomaliza kula chakula walichoagiza ambapo Aretha alionekana kufurahia sana ikiwa Ed ndie alifanya uchaguzi huo, wakainuka na kuondoka. Wakarudi hadi sehemu ya kusubiri huku wakiendelea na maongezi.
Saa moja baadae walikuwa ndani ya ndege ya Malaysia Airlines ambayo ilielekea moja kwa moja Sidney ikiwa ni safari ya masaa nane, Aretha alitazama nje ambapo giza lilitanda japokuwa sehemu kubwa taa zilimulika pale uwanjani na kumfanya aone uzuri wa uwanja huu. Aretha alifurahia kuwepo sehemu hii ya ndege ambayo mara zote alisikia tu sifa zake. 'First Class' kwenye ndege hii ilikuwa bora zaidi na yenye kuvutia. Edrian alitumia muda ule kutazama baadhi ya mambo ambayo yalikuwa kwenye ajenda za kongamano katika kompyuta yake huku mara kadhaa akimtazama Aretha na furaha iliyokuwa wazi kwake.
"Mr Simunge am so glad to see you again" sauti nzito ya kiume ikamshtua yeye na Aretha wakainua macho kumuelekea
Edrian akashtuka kumuona "Mr Job!!". Aretha akamuangalia Ed ambaye alikuwa katika mshangao
"Nilidhani nimekufananisha, lakini niliposogea nikagundua ni wewe, by the way thank you for taking care of repair bill" Mr Job akanyoosha mkono kumuelekea Ed ambaye alitabasamu na kupokea kisha wakasalimiana kabla tangazo la mhudumu kuwakatisha,
"Unaelekea kwenye kongamano?" Akauliza Mr Job
Edrian akatikisa kichwa kukubali, lakini kabla ya kuuliza swali lile lile kwa Mr Job alishtuliwa na swali lililofuata kwa huyu bwana baada ya macho yake kuangukia kwa Aretha
"Your wife ah?"
Edrian akatabasamu na kushika kiganja cha mkono wa Aretha "Yes, she is indeed"
"Ooooh good choice" Mr Job akamwambia kisha akaelekeza mkono kwa Aretha
"Habari yako Mrs Simunge?"
Aretha alishtuliwa na salamu hii, na wakati huo Ed aliuachia mkono wake na kumpa nafasi nzuri ya kupokea salamu kutoka kwa Mr Job. Baada ya kusalimia Edrian akamuuliza ikiwa nae alikuwa njia moja na yeye, lakini Mr Job akakataa..
"Ninafanya kazi chini ya wizara ya Utalii na Viwanda. Naenda Sydney kuwasilisha mpango namba moja wa mkakati uboreshaji wa misitu katika mbuga zetu"
Tangazo la mhudumu likiwaelekeza kujiandaa kwa safari lilimfanya Mr Job awaage na kuelekea kwenye kiti chake.
Wakati haya yakiendelea kulikuwa na mtu hatua chache kutoka walipokuwa akina Ed akijaribu kunasa picha kutoka alipoketi huku akiwa amevaa kofia ambayo ilifunika kwa namna ambayo isingekuwa rahisi kumtambua kwa sura yake.
Mara Mr Job alipoondoka, Ed alifunga mkanda na kuendelea kufunga ule wa
Aretha,
"Unamfahamu huyo bwana?" Akauliza Aretha
"Ndio, juzi nilipata ajali ya gari yangu na ya kwake" Ed akamjibu huku akirudisha kompyuta yake vizuri, mkono wa Aretha ukamshika kwa ghafla
"Ajali!!!, ilikuwaje?" Mshtuko wa Aretha ulikuwa wazi machoni pake, Ed akauangalia ule mkono uliomshika akatabasamu japo aligundua kosa lake kuwa hakumwambia Aretha..
Akaweka mkono wake shavuni kwa Aretha, "Ndio 'princess', nilipata ajali ndogo lakini sikuumia wala gari yangu haikuumia zaidi ya gari ya huyu bwana"
Aretha akamtazama machoni kisha akalaza kichwa chake kwenye bega la Ed... kitendo hiki kilisababisha tabasamu kubaki usoni kwa Ed...
"Rian ilikuwaje?" kwa sauti ndogo ya kunong'ona Aretha akauliza
Edrian akamsimulia namna ajali ilitokea, lakini akamueleza hatua walizofanya kufuatilia gari iliyoingia mbele yake
"Rian, tafadhali naomba uwe unaniambia. Nitajisikia vibaya ikiwa jambo bay__"
Ed akamuwahi na kuweka mkono wake mdomoni kabla ha kuinama na kumbusu juu ya paji lake la uso...
"Mabaya hayatanipata Retha. Asante kwa kuniwazia"
Wakabaki wakiwa wameegemeana kwa dakika kadhaa hadi Ed alipomuona Aretha akiwa amepitiwa na usingizi. Akamtazama usoni kisha akatabasamu na kumuegemeza vyema kwenye kiti..