Harakati za kutaka kujinasua mikononi kwa Ed ghafla zilisitishwa pale alipokumbuka wapi alikuwapo kabla ya kujikuta kitandani..
Akashtuka na kuvuta shuka halafu akajichungulia taratibu "eewhhh" akashusha pumzi na kujifunika hadi usoni....hakutaka kufumbua macho akiwaza hizo nguo ni nani alimvalisha wakati mara ya mwisho alipitiwa na usingizi akiwa bafuni...
"Utajifunika hadi lini?" Sauti yenye mikwaruzo ya usingizi ikamsemesha na kumfanya Aretha ashtuke na kuvuta sana ile shuka.
Edrian akatazama namna ambavyo alimkumbatia Aretha akatamani waendelea kuwa hivyo na wasiamke kabisa. Akakumbuka usiku ule ulivyokuwa wa mahangaiko kwake, maana baada ya kutoka mle chumbani na kwenda kwenye ofisi yake bado hakuweza kulala vyema sababu ya alitamani awepo kitandani kwake ili kuendelea kumtazama Aretha.
"Retha utakosa hewa mpenzi, jifunue" Ed akamwambia huku akijinyoosha, akashtuka kumbe hakuwa na shati maana aliiacha ofisini. Akamwachia kisha akashuka kitandani na kujinyoosha halafu akapiga hatua kuelekea kabatini akavuta fulana akavaa, akarudi na kusimama upande wa Aretha!
"Bafuni upande wa kushoto wa kabati kuna miswaki, jiandae, nguo zinakuja sasa hivi, chai itakuwa tayari nusu saa" alipomaliza kusema akamgusa kichwani huku akiwa amejifunika shuka vile vile kisha akatoka chumbani..
Edrian alijua Aretha anahitaji nafasi, akaelekea kwanza chumbani kwa Coletha, lakini hakuwepo akaamua kushuka jikoni!
Akamkuta Coletha na Zena wakiwa katika maandalizi ya kifungua kinywa, walipomuona Edrian wakamsalimia
"Mmeandaa nini leo?" Edrian akauliza akiwa ameegama kwenye mlango,
Coletha akacheka, "Tuna chai ya maziwa, chapati na maini"
Edrian akatabasamu "mmekamilisha au mnahitaji msaada wangu?"
"Kaka hapana tumemaliza tayari" Zena akajibu huku akipanga vikombe kwenye sinia
"Ooooh basi sawa Zey hataki niingilie ofisi yake, mzigo wangu najua mmeupokea nitaupata wapi?" Akauliza Ed
"Uko sebuleni pembeni ya kochi karibu na Tv" Coletha akamjibu naye Edrian akageuka na kuondoka...
****************
Nusu saa iliyofuata, Edrian alikuwa mezani ameketi huku pembeni akiwa amekaa Aretha ambaye aliinamia sahani yake huku pembeni yake akiwa ameketi Coletha.
"Retha kula usiogope hapa ni nyumbani" Coletha akamwambia
"Aaaahhh sawa nakula Coletha" Aretha akaitikia na kuendelea kula..
Edrian alimwangalia mara kadhaa akifurahishwa na namna ambavyo aliona haya kumtazama usoni.
Muda mfupi uliobaki waliutumia kula kimya huku wakitazamana kwa kuibia.
************
Mida ya saa nne asubuhi, Edrian alikuwa akiendesha gari huku pembeni yake akiwepo Aretha. Safari ilielekea kwenye manunuzi kwa ajili ya safari ambayo ilikuwa usiku wa siku ya Jumanne.
"Huniambii tunaenda wapi Rian?" Akauliza Aretha akiwa anatazama jengo la 'Victoria Fashion and Design' kabla ya kushuka
"Hahahha Subira Retha..vuta subira" akacheka na kumwambia
Wakashuka na kuelekea ndani, Jumapili asubuhi hakukuwa na watu wengi, japokuwa Edrian alishamuandaa V bado aliona vyema kuwahi...
"Rian nguo nilizonazo zinatosha usiongeze nyingi zaidi" Aretha akamnong'oneza Ed kabla ya Victoria kuwasili huku wakiwa wameketi kwenye kochi la wawili sehemu ya kusubiri,
"Aretha, Edrian karibuni sana" V akawasalimia huku akiketi kwenye kochi mojawapo
"Asante sana dada V" Aretha akaitikia
"Tunashukuru V, Asante kwa kunivumilia" Ed akamwambia kwa sababu Victoria huwa haendi kazini siku ya jumapili
"Nashukuru pia kwa kuniunga mkono Ed, nafurahi kuwahudumia" V akajibu kwa uchangamfu mkubwa
"Kila kitu kiko tayari?" Akauliza Ed
"Ndio kaka tunaweza kuanza" akajibu V na kumfanya Aretha kushangaa walitaka kuanza nini
"Tuelekee huku VIP" V akasema huku akiinuka, akifuatiwa na Ed, Aretha akajiunga nao
Aretha akainua macho kumwangalia Ed wakati wakiingia kwenye chumba maalumu cha majaribio ya nguo!
Chumba kilikuwa si kikubwa sana na wala si kidogo sana. Kulikuwa na kochi la watu wawili, meza ndogo, jokofu dogo, kioo kikubwa ukutani huku pembeni kukiwa na pazia lililowekwa kwa mfano wa chumba kidogo ambapo palikuwa sehemu ya kubadilishia nguo. Nguo kadhaa zilikuwa juu ya meza.