Aretha hakuitika bali akafumbua macho akamwangalia kisha akafungua mlango wa gari akashuka. Edrian hakuelewa nini kinaendelea akadhani huenda alimuudhi lakini akatupilia mbali lile wazo sababu aliamini yeye ndie anayehitaji kufahamu kwa nini BM na Aretha walikutana pale. Akashuka kwenye gari na kuelekea mlangoni ambapo Aretha alisimama akimsubiri
Walipoingia ndani wakakutana na Coletha na Zeynabu wakiangalia tamthilia pale sebuleni.
"Rethaaaa!" Coletha akainuka na kumkumbatia Aretha akimkaribisha.
Walipomaliza kusalimiana
"Leo utalala kwetu eeeh?" Coletha akauliza kwa shauku
Aretha akatabasamu na kukubali kwa kichwa kitendo kilichomfanya Coletha afurahi mno.
Edrian akaona awaache akapandisha ngazi kuelekea chumbani kwake. Alipofika akajitupia kwenye kochi kwa uchovu hakuelewa afurahi au awe na mashaka.
"Sijui alipata chakula?" Akawaza
Akachukua simu yake na kumtumia Coletha ujumbe, "Muandalie chakula na chumba chake".
Alipomaliza akainuka na kutoa koti, akajiandaa kueleka bafuni akihisi anahitaji maji baridi kutuliza mwili wake ambao alihisi una joto. Akaelekea bafuni akaiacha simu ikiwa mezani..
****************
"Zey hebu muwekee mgeni chakula" Coletha akamwambia huku akimgeukia Aretha
"Retha ule chakula halafu nikupeleke chumbani kwako au tulale wote?
"Aahm vyovyote tu Coletha nitashukuru" Aretha akajibu huku macho yake yakielekea kwenye ngazi zilizoelekea juu! Akamuuliza Coletha "vipi kuhusu Rian, yeye atakula saa ngapi?"
"H ahhaha big bro anaweza kula au la! Tumeshamzoea anaweza ale au asile japokuwa siku hizi anajitahidi kula"
"Basi naomba nisile kwanza hadi nijue kama tutakula nae" akamwambia Coletha
Coletha akatabasamu "basi sawa ngoja nimuulize." Lakini kabla ya kutoa simu yake akapata wazo ambalo hakika ni sehemu ya mpango wake wa siri. Na kwa kuangalia kama mtu aliyeyasoma mawazo ya Aretha akamshtua "Unataka kuongea na bro kwanza eeeh?"
"Mmmh. ...aahm.." akapata na kigugumizi lakini akakubali kwa kutikisa kichwa
"Hahaha usijali, twende nikupeleke" Coletha akamwambia huku akiinuka.
Aretha akamwangalia kwa wasi wasi, "Usiogope mwaya, bro ni bonge la mstaarabu" Coletha akamwambia huku akimshika begani
Aretha akainuka na wakafuatana na Coletha wakapanda ngazi. Walipofika juu walikatisha kuelekea upande wa kushoto tofauti na siku aliyokuja kwa mara ya kwanza. Wakaendelea mpaka walipofika kwenye mlango wa chumba cha Edrian.
"Mgongee, ukiona kimya anaweza kuwa kapitiwa na usingizi" Coletha akamwambia kisha akamwacha akaelekea chumbani kwake kuandaa mazingira ya mgeni.
Aretha akabaki amesimama kisha akashusha pumzi na kugonga mlango taratibu...
Sekunde kadhaa zilipita pasipo mlango kufunguliwa wala kusikia akiitikia . Aretha akaamua kufuata ushauri wa Coletha, akafungua taratibu na kuchungulia ndani ambapo mandhari ya chumba ilimvutia kiasi cha kujikuta akiwa akapiga hatua kuingia ndani huku akirudisha mlango taratibu.
Akaangalia rangi zilizopakwa ukutani kwa namna ilivyoendana na rangi ya samani zilizomo mle ndani. Rangi ya jivu yenye utepe mweupe iliendana vyema na kabati na meza nyeupe. Akiwa amesimama huku macho yake yakishangaa, kitasa cha mlango kilisikika kikifunguliwa. Mlango ukafunguliwa na Edrian akatokea huku akiwa amefunga taulo kiunoni
"Retha" Edrian akashangaa kumuona mtu chumbani kwake akabaki akiwa amesimama wima pale alipokuwa wakati huo Aretha alipatwa na mshangao mkubwa asijue aende wapi.
Edrian akapiga hatua na kumsogelea Aretha ambaye sasa aliinua uso kumtazama huku akili yake ikimwambia ageuke kuondoka lakini macho yake yalipata ushawishi wa kuendelea kuangalia mwili wa Ed. Hakujua saa ngapi Edrian alimfikia, akamshika mkono wake akionekana kabisa alikuwa katika ulimwengu wa ndoto. Ule mguso wa mkono ulimrejesha kwenye fahamu zake.
Alipokaza kumtazama Edrian, ghafla machozi yakaanza kutiririka taratibu kwenye mashavu ya Aretha. Kitendo kile kikamshtua Ed, "Retha kwa nini unalia" akamwangalia usoni lakini hakupewa jibu isipokuwa Aretha akamkumbatia kwa ghafla
"Ooooh Rian nisamehe sana, sikujua ingekuwa hivyo" maneno haya yaliambatana na kwikwi za kulia