Renatha alikuwa wa kwanza kubomoa ngome ya Allan, lakini baada ya muda walibaki kwenye sare ya sitini na tisa. Wakasimama kila mmoja akitweta, ilikuwa wazi kabisa kila mmoja alikubali uwezo wa mwingine.
"Kwa hali ilivyo tunaamuaje Renee?" Allan akauliza huku akiinama mikono yake ikiwa kwenye magoti..
Renatha ambaye aliegemea kwenye mpini ulioshikilia goli akainuka, "tucheze dakika kumi za mwisho" akasogea huku akiurusha mpira kumwelekea Allan ambaye aliudaka. Akatabasamu
"Naona unachotaka ni cha muhimu hutaki yaishe" Allan akamtania
"Hahaha siwezi kukuachia kwa urahisi hivyo" Renatha akajibu huku akimsogelea Allan tayari kukaba mpira..
Mtanange kati yao ambao ulikuwa hauna mashabiki wala yoyote aliyeusimamia ulianza. Sasa nguvu pia ilitumika mara kwa mara Renatha alimchezea vibaya Allan lakini yeye alitabasamu na akaendelea.
"Amechoka na hataki kushindwa!!" Allan alimshangaa Renatha. Hakutaka kupoteza mchezo huu, alitaka kujua hasa kusudi la Renatha kutaka kuwa karibu na Edrian. Japo alishawishika kuwa ni hali ya kawaida kwa baadhi ya wanawake kujaribu kumpata Ed, lakini sasa kwa namna alivyomuona akicheza aliamini kuna sababu zaidi ya kumpenda tu Ed. Akaamua maamuzi ambayo alijua yatagharimu.
Wakati Renatha akijaribu kumkaba ili kuupokonya mpira, Allan akateleza na ikawa ni sekunde ambayo ilimpa ushindi Renatha.
"Nimekushinda" Renatha akasema huku akimrushia mpira kwa nguvu Allan ambaye alikuwa ameinama, mpira ukamgonga begani
"Ooouch" Allan akalalama
Renatha akiwa tayari amegeuka kuondoka aliposikia sauti ya Allan akilalamika akageuza shingo, akamuona akiwa ameshikilia bega lake
"Samahani Allan" akapiga hatua za haraka kusogea pale alipokuwa Allan ambaye alipoona wasi wasi wa Renatha akakunja uso kabisa
"Umeamua kuniumiza kabisa" akaongea kwa kudeka
"Aaargh...sijafanya makusudi.. acha kudeka" Renatha akamuinua kisha akavuta mkono wa Allan kwa ghafla
"Aaaaaahh"
"Hey Mr Nubri hupendezi kudeka" Renatha akamwambia kisha akaanza kupiga hatua kuelekea nje ya uwanja
"Haaaaaa, kudeka!! Ukinidekeza nitadeka" Allan akapiga hatua nyuma yake huku akichukua begi lake lililokuwa kwenye benchi la mbele...
"Hey Renee nisubiri, umeniumiza bega langu hata kunisaidia hutaki!!" Allan akamuita Renatha
Renatha hakusimama lakini akapunguza mwendo kiasi cha kufikiwa na Allan akanyoosha mkono kumuelekea akimaanisha apewe begi
Allan akampa, japo alitamani asimpe maana Renatha alikuwa na mfuko uliobeba nguo zile ambazo alikuja amevaa, akaamua kubaki na mpira
"Niambie ombi lako maana umeshinda kihalali" Allan akamwangalia huku tabasamu lake likiendelea kubaki usoni na wakawa wakitembea kuelekea mahali gari liliegeshwa
"Niandalie chakula cha jioni na Mr Simunge"Renatha akamjibu
"Ahaaaa hivyo tu?" Allan akajifanya kushtuka
"Au ulidhani nitakuomba kingine?"Renatha akauliza
"Haha hapana, ila kwa nini? Unampenda?" Allan akasimama ghafla na kumwangalia Renatha ambaye naye alishtuka na kumuangalia
"Utafanya au unataka tukubaliane mchezo mwingine!
"Eeeeh unapenda kucheza kamari?" Allan akamuuliza huku wakisogea mahali walipoegesha gari.
Renatha hakumjibu akaendelea kutembea na mwishowe akasimama kwenye mlango wa gari. Allan akabofya ufunguo na milango ikawa tayari kufunguliwa. Yeye akaelekea mlango wa dereva na kutaka kuingia lakini alishangazwa na kuona Renatha ameketi tayari kwenye kiti cha dereva, akamnyooshea mkono ampe funguo, naye akafanya hivyo kisha akazunguka na kuketi.
Safari ya kurudi ikaanza, dereva hakutaka kupoteza sekunde barabarani kwa mwendo walioondoka nao.
"Renee una hakika hautaharibu gari yangu kwa hii spidi" Allan akauliza huku akimtazama pasipo shaka usoni lakini moyoni mashaka yalikuwa makuu.
"Jumamosi saa mbili Golden Hotel. Utaweza au niigonge kwenye lori ununue jingine au tusiwepo duniani " Renatha akamwambia huku akikwepa gari iliyokuwa ikielekea usawa wao
Allan akamwangalia Renatha ambaye uso wake ulioelezea hakika ya kile alichokisema. Akarudisha macho yake akaona Lori ambalo lilikuja mbele yao na Renatha alikuwa katika mraba usio wake
"Basi sawa Renatha" Allan akahamaki