Aretha akiwa amepatwa na butwaa kuona kile kilichotokea kwa ghafla, mkufunzi kwa kutumia kipaza sauti akawaita Charlz na Bruno mbele. Akazungumza nao kisha wakatoka darasani, minong'ono ya hapa na pale ilisikika mpaka mkufunzi alipowanyamazisha na kuendelea na darasa.
Kwa upande wa Aretha, hakuwa tena na utulivu kufuatia tukio lile. Alimwangalia mwalimu lakini mara kadhaa akipitwa na kile kilichofundishwa. Akatoa simu yake kisha akamtumia ujumbe mfupi Charlz kumuuliza yuko wapi.
Kimya kiliendelea kwenye simu ya Aretha pasipo majibu yoyote kutoka kwa Charlz. Akaendelea kutazama alipokuwa mkufunzi hadi alipomaliza na bado hakuwa amepata ujumbe wowote kutoka kwa Charlz. Mara mkufunzi alipotoka, Aretha akakusanya vitu vyake na kuweka kwenye begi kisha akisimama ili kutoka lakini akajigonga mbele ya mtu
"Hey unawahi wapi wewe?" Akaongea kwa dharau huku akimwangalia kwa chini kutokana na kupishana kwao urefu
"Samahani" Aretha akamwambia huku akijaribu kumpita lakini yule kijana akasogea na kumzuia
Ghafla wakasogea mahali pale watu wachache ambao bado walikuwa wakitoka taratibu
"Kuna nini kwani?" Mmoja kati ya watu waliosogea akauliza huku macho yake yakimtazama Aretha kisha yule kijana
"Hakuna kitu, mind your business" akajibu kwa ujeuri huku akisogea kidogo kukabiliana na yule aliyeuliza
Aretha akatumia mwaya huo kutoka nje akatembea haraka kuelekea jengo la utawala huku akipiga simu ya Charlz. Simu ikaendelea kuita pasipo kupokelewa..
Akaingia mapokezi na kuuliza ikiwa Charlz alifika kumuona 'Dean of students' lakini akaambiwa hawakufika. Na wakati huo akamuona mkufunzi aliyemaliza kipindi darasani kwao akiingia na kuulizia lakini alipata majibu yale yale.
Aretha akawaza kuelekea karibu na hosteli ambayo Charlz anaishi. Eneo hilo kulikuwa na miti mingi iliyopandwa njiani. Wakati Aretha akielekea kule mtu mmoja alikuwa akikimbia nyuma yake. Lakini alipomkaribia akamshika mkono kama mtu aliyehitaji msaada wake wa haraka.
Aretha alipoinama kutaka kumshika mkono yule mtu akainua mkono na kumfunikia na kitambaa laini na hakuelewa nini tena kilichotokea.
*****************
Edrian alikaa kwenye kiti akiendelea kusoma na kutoa maoni yake kwenye tathmini aliyokabidhiwa na Renatha. Akaangalia simu yake akitaka kuandika ujumbe kwa Aretha lakini akasita, "ngoja nimpe muda maana jana hakwenda chuo" akawaza Ed.
Mchana akashindwa kusubiri akaamua kupiga simu ya Aretha. Simu ikaita kwa muda mrefu pasipo kupokelewa.. Ed akapata wasi wasi akampigia Charlz, simu yake nayo ikaita muda mrefu na haikupokelewa.
Alipoona hivyo akampigia Captain kumuomba amsaidie kujua alipo Aretha kwa kufuatilia ishara ya mnara iliposoma mara ya mwisho. Captain alipotazama akagundua kuwa mahali simu ya Aretha ilipo ndipo ambapo namba ile ilimpigia Ed usiku wa jana ilikuwepo.
Ed sasa alikuwa kwenye gari akielekea maeneo ya chuo lakini hasa kwenye nyumba ambayo ilioonesha simu ya Aretha ipo. Wakati huo akampigia simu Derrick kumuomba awatafute rafiki walio karibu na Charlz ila wajue mahali alipo.
"Please Aretha be safe" akawaza Ed huku mwendo wa gari ukiongezeka pasipo kujali. Akampigia Allan kumpa taarifa ya kusimamia majukumu yake. Akaendelea kuipiga simu ya Aretha lakini bila mafanikio ya kupokelewa.
Mara alipofika kwenye ile nyumba mahali ambapo simu ya Aretha ilionesha kuwepo, akashangazwa na kukuta geti likiwa wazi. Alipoingia ndani ya geti akaipiga simu ikasikika kutokea ndani akaamua kufuatilia kwenye mlango ambapo alisikia.
Alipofungua mlango akasikia sauti nyingine ya mtu ambaye aligonga mlango kutokea ndani ya chumba ambacho ilikuwa ni stoo. Akapiga hatua za taratibu kuelekea kule sauti ilisikika..
"Tafadhali nisaidie, nifungue sitajaribu kusema mambo yasiyonihusu" sauti ile ililalamika. Ed akaamua kufungua sababu alihisi kuifahamu sauti hii, macho yake yakakutana na dada ambaye mikono na miguu yake ilifungwa kwa nyuma kwenye kiti alichokalia , alionekana kuchoka sana huku nywele zikiwa zimevurugika.
"Afadhali umekuja kunisaidia Ed" akasema kwa shida huku akimwangalia Ed amfungue mikono na miguu
"Mbona uko hapa?" Ed akamuuliza