Chapter 157 - MSHTUKO

Aretha alichungulia kupitia mlango uliokuwa karibu na mlango mkuu wa kuingia ukumbini, akabaki kujifinya vidole vyake woga as ghafla ukimpata. Idadi ya watu waliokuwa nje ilimfanya apatwe na wasiwasi iwapo angetakiwa kuongea chochote.

"Retha, relax princess" Edrian akasogea kwa nyuma huku akimgusa taratibu kwa mikono yake ambayo kwa wakati huo ilikuwa faraja kuu kwa Aretha, akajikuta akiegama ubavuni mwa Ed. Derrick aliyekuwa hatua chache kutoka walipokuwa alitabasamu kwa kile alichokionà.

Dakika chache baadae waliingia ukumbini, kwa wakati huo picha zilizungushiwa kitambaa mfano wa pazia na kuzifanya zisionekane. Beruya alishika kitufe ambacho mara tu atakapo bonyeza basi kitambaa kile kingefunguka taratibu na kuacha picha zionekane.

Beruya akasimama kwenye jukwaa ndogo, alivalia gauni ya rangi ya dhahabu refu huku nyuma yake lilibeba nakshi za kuvutia na nywele zake zikiachiliwa hata kumwagika upande mmoja. Akasimama mbele ya kipaza sauti na kuzungumza

"Ndugu mabibi na mabwana, nachukua fursa hii kuwakaribisha kwa furaha kwenye onesho la B- Hands, ambalo leo litakupa nafasi ya kuona uchoraji asili. Kila picha inabeba hadithi au historia kwa nini na kwa nani ilikusudiwa kwenda." Akameza mate taratibu kisha akaendelea

"Na onesho la leo litabeba simulizi za wachoraji wawili katika picha. Nina mwenzangu ambaye atawaletea ladha yake katika uchoraji. Kama ninavyosema mara zote "mikono yetu hueleza mioyo yetu". Nawaletea kwenu mkono wa binti mchanga lakini hodari kama mzee kwenye mikono yake." Akanyamaza na kumuangalia Aretha aliposimama, akaendelea

"Makofi kwa Aretha Thomas" Beruya akaendelea huku makofi yakipigwa na taa ikammulika Aretha ambaye alisimama karibu sana na Edrian.

Mwanga ule ulimfanya Aretha afumbe macho mara kabla ya kuyafumbua tena. Hii ni kwa sababu taa za mle ndani zilipunguzwa mwanga kiasi cha kufanya hali ya ukumbi kuwa kama usiku na kumbe ilikuwa alasiri.

Beruya alipomaliza kuwakaribisha wageni na kutambulisha baadhi ya simulizi zilizo ndani ya picha zitakazooneshwa mle ndani, wakati wa kufungua utepe wa onesho uliwadia. Akamuita Aretha kufika pale jukwaani ili waweze kubonyeza kitufe cha ufunguzi.

"You can do this princess" Ed akamnong'oneza Aretha mara alipoona kusita kwake

Aretha akapiga hatua na kusimama jukwaani akiwa na Beruya. Watu wakahesabu kurudi nyuma kuanzia kumi hadi moja kisha mikono yao kwa pamoja ikabonyeza kitufe na pazia likajivuta lenyewe na kuziachia wazi picha. Ghafla makofi yaliyokuwa yanapigwa yakapungua na macho ya watu yakashangaa huku sauti zikianza kupishana kila mmoja akiongea kwa mashaka....

'What is this'

"Mambo gani haya sasa"

Lakini watu walipokuwa wakishangaa, Beruya alipatwa na mshtuko mkubwa na kabla ya kufanya chochote akainama kujaribu kujiweka sawa lakini akashindwa na kuanguka chini. Kitendo kile kilimshtua zaidi Aretha ambaye aliinama kujaribu kumsaidia Beruya akamuita lakini hakuweza kumjibu bali alibaki ameshika kifua..

Ndani ya sekunde chache Edrian na Derrick walipanda jukwaani wakimuita Aretha ambaye alikuwa akijaribu kumsaidia Beruya.

"Tunahitaji Daktari" Edrian akasema kwa sauti huku akifungua kifungo cha koti lake.

"Derrick mchukue Retha tafadhali" Ed akampa agizo wakati huo yeye akimuweka Beruya vyema, ndani ya kundi lile la watu pale ukumbini wakapanda watu watatu na kujiunga nae ambao walionekana ni madaktari. Mmoja kati yao alionekana kumfahamu Beruya

"Nitamsaidia kutokea hapa, naitwa Damian ni daktari lakini ni mchumba wa Beruya, gari ya wagonjwa inakuja sasa hivi" akajitambulisha mmoja kati yao ambaye alionekana kuwa na wasi wasi sana kwa hali aliyokuwa nayo Beruya. Edrian akashukuru moyoni maana jengo hili lilikuwa karibu na City Hospital. Edrian akainuka wakati wale watu watatu wakaendelea na hatua za kumsaidia Beruya

Derrick akafanikiwa kumsogeza pembeni Aretha ambaye alikuwa bado kwenye mshangao wa nini kilikuwa kinaendelea maana kila alichoona kwa macho yake kimetendeka kwenye picha zilizokuwa wazi ndani kilimfanya moyo wake ugande kama barafu.

"Aretha uko salama?" Akauliza Coletha huku akimpa maji pale alipoketi kwenye kiti.