Chapter 155 - MY LOVE

Ilichukua masaa mawili kwa Aretha kumaliza huduma zote ambazo Victoria aliagizwa afanyiwe. Na sasa Aretha akatoka ngozi yake ilionekana kama ya mtoto mchanga.

"Asante dada V" Aretha akamwambia

"Hahaha hata usijali Aretha, hiyo ni shukrani yangu kwa kunibania siri yangu kwa Edrian"

Victoria akamsindikiza mpaka kwenye gari iliyomleta

"Dada V hata usingesumbuka" akashangaa kwa ukarimu wake sababu hakujua kama Victoria ndiye aligharamia, alidhani ni Edrian

"Aretha watu wa "Make Up" wanakusubiri tayari nyumbani" V akamwambia

Aretha akashtuka akijiuliza waliwezaje kufika, Victoria akamuondoa shaka

"Usishangae 'dear', huyu dereva aliyekuleta ndio amewapeleka walihitaji muda wa kuandaa mazingira. Mama amewapokea vyema."

Aretha akatabasamu kwa aibu na kumshukuru Victoria..

"Haya muondoke sasa wasije wakanisumbua" Victoria akamfungulia mlango wa gari Aretha na kisha akafunga. Akampa ishara ya kumruhusu kuondoka dereva ambaye ndiye alimleta swali Aretha.

******************

Edrian baada ya kupata kifungua kinywa asubuhi ile aliingia kwenye ofisi yake iliyo katika nyumba yake. Akaendelea kupitia ripoti za uendeshaji wa migodi kwa siku mbili. Akapokea simu iliyoita na kusababisha ahamishe macho yake kutoka kwenye kompyuta..

"Hellow Derrick"

Upande wa pili alikuwa ni Derrick ambaye waliongea kuhusu ratiba ya Aretha na iwapo kutafanyika ununuzi basi yeye atahusika. Walipomaliza, akaangalia saa yake kisha akampigia Aretha lakini simu ilipo pokelewa muungurumo wa mashine ulisababisha kutokusikilizana. Akakata simu na alipowaza kutuma ujumbe tayari Aretha akamtumia

"Sorry Rian, nitakupigia tukimaliza"

Akatabasamu huku akivuta taswira ya muonekano wa Aretha ikiwa amevaa gauni ile aliyoichagua. Akachukua simu na kuangalia ile picha aliyokuwa akipima nguo.

"Wait for me my love am coming to see you" akawaza huku akiangalia saa yake ambapo ilibaki saa moja aende kumchukua Aretha. Akampigia Li kuona kama atapenda kuungana naye japo alijua mara nyingi jumapili hupenda kutumia muda wake na Allan. Akajua ataondoka na Coletha ambaye aliamka na kwenda saluni kutengeneza nywele zake ili kuhudhuria onesho la Aretha.

****************

Mama yake Aretha akamwangalia binti yake asiamini kile alichokiona, huku akijaribu kuzuia macho yake kutokwa machozi akamwambia Aretha aliyesimama mbele yake

"Retha, umependeza sana mwanangu"

Aretha akatabasamu japokuwa kulikuwa na chembe za huzuni ndani yake, "Asante mama, lakini kwa nini tusiende wote mama"

"Shhhhh! Usiweke huzuni kwenye uso wako. Uwe na hakika kuwa nitakuja onesho lako la kwanza. Nitabaki kukuombea kwa Mungu binti yangu"

Aretha akashusha pumzi na kukubaliana na mama yake.

"Umependeza sana jamani" Coletha akamwambia huku ndani shauku yake ni ule mshangao utakaompata kaka yake ambaye alibaki nje akiwasubiri baada ya dada yake kumzuia asiende

Edrian aliinama kwenye usukani wa gari akijizuia shauku yake ya kutaka kuingia ndani. "Kaka hebu subiri nikaangalie kama yuko tayari si unajua mambo yetu kina dada" akayakumbuka maneno ya Coletha

"Aaaaaargh huyu nisingekuja naye tu" akawaza na mara akasikia kitasa cha geti kikifunguliwa akainua uso wake akitegemea kumuona Aretha lakini matarajio yake yakazamishwa mbali. Mama yake Aretha akatoka getini, alipomuona akafungua mlango na kushuka chini

"Mama" akaita kwa heshima huku akipiga hatua kumsogelea

"Mwanangu, Coletha kaniambia amekuzuia usije eeeeeh!"

Edrian akacheka huku akitikisa kichwa kukubali

"Hawa wasichana wana mambo" Mama akatania lakini macho yake yalitoshelezwa na muonekano wa Edrian. Alikubali moyoni kuwa Edrian hakika alionekana nadhifu na mwenye mvuto mkubwa...

"Mwanangu kama tulivyoongea kwenye simu sitakuwepo lakini ninaweka imani yangu yote kwako. Nashukuru na naamini hatua hii itazaa safari nzuri kwake. Kila la heri." Mama akamwambia Edrian kisha akaita kwa sauti "Coletha"

Geti dogo likafunguliwa huku Coletha akitangulia kisha Frans aliyevaa suti ya rangi ya bluu iliyokolea akafuata kwa nyuma. Aretha akafuatia nyuma ya Frans, macho yake yalihama chini kwa aibu ya kuogopa kuonana na macho ya Edrian.