Chapter 132 - MNUFAIKA

Edrian alihakikisha hatua zake zinafuatana na zile za Aretha ili asionekane kama anamkokota. Walielekea mpaka kwenye mlango wa kuingia benki ya Golden, mahali ambapo ungekutana na wafanyabishara wakubwa.

Kwa upande wa Aretha hakuelewa kabisa kwa nini walikuwa mahali pale. Hakuwahi kuingia katika benki hii kwa kuwa katika mji huu iliheshimika kwa hadhi ya watu walioitumia. Wakati Edrian alipomshika mkono mapigo ya moyo wake yalienda mbio. Akajaribu kuituliza akili yake ambayo ilisambaa kuangalia watu waliokuwa nje ambao ukweli waliibia kuwaangalia.

Edrian alisukuma mlango, wakaingia na kuelekea moja kwa ofisi ya Meneja wakiwaacha watu wachache waliokuwa wakihudumiwa kwenye ukumbi wa Benki hii.

"Habari ya mchana Fatma" Edrian akamsalimia dada ambaye alionesha kumezwa na kazi aliyokuwa nayo kwenye Kompyuta iliyokuwa mbele yake.

"Oh, karibu Mr Simunge samahani sikukuona wakati unaingia" dada huyu alisimama kumsalimia Ed huku macho yake yakimwangalia Aretha na kushuka kwenye muunganiko wa mikono yao

"Hapana shida Fatma. Chris nimemkuta nilikuwa na miadi naye"

"Ooh yupo Mr Simunge. Namtaarifu uwepo wako mara moja"

"Habari yako dada" Fatma akamsalimia Aretha ambaye alikuwa akijaribu taratibu kujichomoa kwenye mkono wa Edrian lakini hakuweza maana kila alipojaribu ndio ulishikwa zaidi.

"Ah salama" akaitika.

Baada ya kujulishwa, akaruhusiwa kuingia. Edrian akiwa na mkono wa Aretha bado waliingia ofisi ya Meneja wa benki hii ya Golden.

"Aaaaah Mr Simunge karibu" Meneja Chris alisimama na kunyoosha mkono akimkaribisha ofisini kwake.

Edrian akaachia mkono wa Aretha na kusalimiana na Meneja, Aretha alikangalia mandhari iliyomvutia ya ofisini mle..

"Hii ofisi daah" akawaza

"Chris huyu ndio Aretha" Edrian akamtambulisha. Chris akanyoosha mkono na kumsalimia Aretha huku akiwakaribisha kuketi.

Akabonyeza simu yake "Fatma nitumie fomu za Aretha Thomas"

Aretha akashtuka na kumwangalia Edrian ambaye hakuonesha mashaka yoyote.

"Nimefanyia kazi hatua zote kama ulivyoagiza tumebakiza sehemu ya uthibitisho wake na akaunti itakuwa tayari kutumika kuanzia sasa." Meneja Chris akamwambia Edrian ambaye aliitikia kwa kichwa kuonesha furaha yake kwa kile wamefanya.

Aretha akajaribu kumuangalia Edrian akitegemea walau atapewa taarifa walau fupi lakini Edrian alikuwa akimsikiliza Chris. Aretha hakuelewa maana alikuwa ana hakika kuwa hakuhitaji akaunti nyingine. Kwa mwanafunzi wa chuo ilikuwa ni lazima kuwa na akaunti ya Benki.

Akaunti Golden Bank bado ilikuwa ni mchanganyo katika akili ya Aretha. Gharama ya kufungua akaunti ilikuwa ni mtihani kwa mwanafunzi kama yeye. Lakini kuwa na akaunti hapa ni dhahiri lazima uwe mtu mwenye mzunguko mzuri kifedha ili kukupa nafasi pia ya kufaidika na mikopo yao iliyosemekana kuwa na urahisi wa Riba.

"Okay, Aretha Thomas umefunguliwa Mnufaika akaunti (Beneficiary Account), akaunti hii itakupa wewe kutumia kiasi cha fedha ambazo zitakatwa kutoka katika akaunti ya mmiliki aliyekufungulia akaunti kwa kila mwezi.

"Eeeh!" Aretha alishtuka huku akirudisha macho yake kutoka kwa Meneja Chris hadi kwa Edrian lakini alikutana na tabasamu.

"Ndio Aretha, utanufaika kutoka kwenye akaunti ya Mr Simunge kila mwezi kwa asilimia 25 ya mapato yake atakayoingiza kwenye akaunti yake. Hivyo kadi yako iko hapa, nahitaji tu uingize alama yako ya kidole kwenye mashine hii na utaanza kuitumia akaunti mara moja."

"Rian" Aretha alimwangalia Ed ambaye wala hakuonesha shaka bali uso wake ulikuwa na tabasamu

"Retha fuata maelekezo ya Meneja"

Aretha akashusha pumzi na kuweka vidole vyake kwenye mashine huku akimwangalia Edrian ambaye muda huu alishika simu yake akiangalia.

"Asante Aretha. Maelekezo yote ya namna ya kutumia akaunti hapa Golden Bank yatatumwa moja kwa moja kwenye simu yako kwa njia ya whatsapp. Asante sana na karibu Golden Bank, Your Money is safe always." Meneja Chris akamkaribisha Aretha

"Nadhani tumemaliza meneja?" Edrian akamuuliza Meneja

"Oooh yes Mr Simunge. Asante kuiamini Golden Bank." Akashukuru Meneja

Edrian akainuka na kushikana mikono na Meneja "Asante sana kuiamini SGC Chris.