Edrian alisimama nje ya geti la nyumbani kwake akimsubiri mlinzi ambaye alifungua geti kuruhusu gari kuingia ndani. Njiani kote alitafakari kwa namna gani atamsaidia Aretha ili kazi yake ya uchoraji ifahamike na kumuingizia kipato. Aliwafikiria baadhi ya watu ambao wanaweza kuwa msaada wa karibu kwa Aretha. Aliongea na Derrick ambaye hupenda kuhudhuria kwenye matukio yanayohusiana na uchoraji kwa kuwa kuna uhusiano mkubwa na shughuli ya Utalii ambayo ilikuwa kwenye malengo yake.
Alikusudia kuwatafuta baadhi ya hao watu siku itakayofuata na kuona namna ambayo wanaweza kumpa hamasa Aretha. Alitabasamu alipomkumbuka Aretha akageuka na kuangalia ile picha aliyoiweka nyuma. Shauku yake ya kuona ni nini Aretha alikichora ikaongezeka zaidi.
Akaendesha kuelekea ndani baada ya mlinzi kufungua geti. Kama ilivyo kawaida yake akamsalimia na kuelekea kwenye maegesho. Kwa muda aliofika alijua Coletha atakuwa amekwisha pumzika na kwa upande wa Li alijua atakuwa sebuleni. Akashuka na kuchukua picha yake kisha akapiga hatua kuingia ndani.
Mara alipofika kwenye sebule, Ed alipokelewa na mtu ambaye hakumtaraji kuwepo nyumbani kwa muda ule.
"Babe karibu" aliinuka Lyn na kuelekea aliposimama Ed. Sauti yake iliashiria hasira
"Unafanya nini hapa Lyn?" Aliuliza Ed huku hasira zikiwa wazi
"Edrian, na mimi nikuulize unatoka wapi saa hii?"
Kabla Ed hajajibu Li alishuka kwenye ngazi akitokea chumbani kwake,
"Za jioni Bro" akawahi kusalimia
"Salama Li" Ed akaitika na kuanza kupanda ngazi kuelekea ilipokuwa ofisi yake ya nyumbani.
Li akajua kwa hali ile ilivyo mambo yatakuwa magumu kwa usiku ule. Aliporejea kutoka kazini Joselyn nae alifika pale nyumbani akionesha wazi hakuwa katika hali nzuri. Alipomaliza kusalimiana akajaribu kumdodosa kujua kama kulikuwa na shida yoyote lakini Joselyn hakusema bali alimwambia Edrian kamwambia amsubiri pale nyumbani. Kitendo cha kusikia ni kaka yake ndie aliyemwambia Lyn hakuona umuhimu wa kumtafuta amuulize. Lakini kwa namna alivyowasikia wakijibizana alijua Lyn alimhadaa.
Ed akaelekea ofisini, Joselyn nae alimfuata nyuma. Naam mara tu alipoingia akaiweka picha kwenye meza na akageuka ili kukabiliana na Lyn ambaye alimuwahi
"Unadhani utanidanganya Ed eeeh!"
"Mmmmmm" Ed akaguna na kumwangalia usoni
"Unatoka kumuona yule mwanamke, hivi amekufanyia nin__"
"Unataka nini hapa Lyn?" Ed akamkatisha
"Nataka uniambie kwa nini ulienda kwa yule mwanamke Ed wakati unajua wiki hii unanivalisha pete au unataka ni__"
Uvumilivu wa Ed sasa ulianza kuyeyuka taratibu "Nani alikwambia nakuvalisha pete Lyn?"
Kabla Lyn hajajibu Ed akaendelea "Ninawajibika kukwambia nani nakutana nae kila siku?" Akamuuliza huku mitetemo ya hasira ikiwa kwenye sauti yake.
"Ed babe nilikwambia yule mwanafunzi sitaki kumuona akikukaribia au uki_"
"Wewe kama nani kunipangia hivyo?" Akauliza akiwa ameegama kwenye meza
"Unataka kujua mimi ni nani Ed eeeh! mimi ndie mwanamke pekee mwenye haki ya kuwa na wewe, unaelewa?" Lyn akajibu kwa jeuri...
"Sikia Lyn, naomba uondoke, rudi nyumbani" Ed akamwambia kwa msisitizo
"Siendi Ed, huyu mwanamke anakudanganya ili uniache eeeh, umeenda kumfuata chuo najua halafu kakupatia na hiyo picha!"
Ed akshtuka kusikia maelezo ya Lyn akamtolea macho akitamani kumuwasha makofi kwa tabia yake ya kumfuatilia ambayo hakuipenda...
Joselyn akasogea aliposimama Ed akataka kuivuta ile picha, mkono wake ukadakwa kwa haraka. Ed akamsukuma nyuma.
"Joselyn kwa mara ya mwisho naomba uondoke, nadhani sihitaji kujieleza kwako kwa namna yoyote" Ed akajibu na kuegama tena kwenye meza
"Huna cha kujieleza eeeh, umesharogwa na hizi picha hata huoni shida kunidanganya" Lyn akasogea tena aliposimama Ed na wakati huu akajaribu tena kusogea ilipokuwa picha kwa kutumia nguvu.
"Joselyn" Mtetemo wa sauti ya Ed ulikuwa kama radi imepiga ghafla mule ndani lakini bado haikumshtua Lyn ambaye alitaka kwa hakika aishike ile picha
Ed alipoona Lyn anakusudia kuivuta ile picha akamshika kwa nguvu na kumbana mikono yake kwa nyuma "Nakwambia Lyn usinijaribu. Go home now"
Lyn akaugulia maumivu kwenye mishipa ya mikono.