Chereads / Tafadhali, Nipende(Please, Love me) / Chapter 118 - NAKUAHIDI

Chapter 118 - NAKUAHIDI

Edrian akampa ishara amsogelee baada ya kuona mama akielekea jikoni. Aretha akamsogelea na kuinama alipokuwa ameketi

"Ni kweli sijala princess."

Aretha akashtuka na kumwangalia usoni, lakini kabla hajamuuliza kwa nini hakumwambia Ed akamuwahi

"Nilikuwa 'busy' kuhakikisha unakuwa salama nikasahau kula"

"Rian unamaanisha au___?" Kikohozi laini kilisikika nyuma yao. Alikuwa Frans aliyelekea kuketi kwenye kiti upande mwingine wa meza. Aretha akainama kwa aibu akaelekea jikoni huku akijaribu kuficha tabasamu lililokuwepo usoni kwake.

"Uko likizo Frans?" Edrian akaanzisha mazungumzo na mdogo wake Aretha wakati wakisubiri chakula kiandaliwe pale mezani.

Mazungumzo yao yalielekea kukolea hadi pale mama na Aretha walipoleta chakula. Wakashiriki chakula pamoja kwa furaha huku mara zote Aretha alijaribu kukwepa maswali ya mama yake yaliyomlenga yeye.

Baada ya chakula, Edrian aliagana na familia hii ya Aretha, wakiwa wamekubaliana na Frans kuwa angeonana nae wiki inayofuata kwa ajili ya kupata mafunzo kwenye utaalam wa mifumo ya mawasiliano.

"Retha humsindikizi mwenzio!" Mama akamuuliza Aretha aliyekuwa amesimama pembeni yake.

"Aaarrrgh mama jamani" Aretha akamwangalia mama yake aliyekuwa akitabasamu, akaelekea aliposimama Edrian na Frans ambaye alielekea nje kuangalia mahali gari ilipoachwa.

"Rian" Aretha akamuita

"Niambie Princess"

Aliposikia hivyo Aretha akainama kwa aibu na kusahau kama Ed alikuwa akisubiri kusikia kile alichoitiwa.

"Retha" akamuita

"Aaahm. .nilitaka upite studio yangu uchukue ile picha nilikuahidi kama hutojali." Akaongea taratibu huku akibinya vidole vyake

"Sawa Princess, am not in hurry" Edrian akajibu kisha akamfuata Aretha hadi kwenye studio yake. Walipoingia Aretha akaelekea kwenye ile picha ambayo ilifungwa vizuri na kuegemezwa kwenye ubao wake.

Edrian aliangalia kazi za Aretha alizochora macho yake yalijawa na mshangao kwa uzuri na ubora wake. Haikukaa akilini kwake kuwa kazi bora kama zile zilitunzwa mle ndani pasipo kutafutiwa wateja.

"Ulishawahi kufanya mnada au maonesho ya kazi zako Retha?" Akauliza akiwa amesimama kwenye mojawapo ya picha iliyokuwa pembeni.

"Hapana Rian. Nadhani bado sijafikia kwenye hadhi hiyo" akajibu Aretha akinyanyua picha tayari kumkabidhi Ed.

"Nani alimwambia hivyo princess?" Akauliza Ed huku akielekea kumpokea Aretha ile picha iliyofungwa vyema kwa karatasi ngumu. "Asante Retha"

"Haaa hapana. Nafikiri bado hazijakaa sawa Rian" akajibu huku akielekea mlangoni

Edrian akatamani aendelee kubaki akiangalia zile nyingine zilizofunikwa, lakini ikamlazimu kumfuata nyuma Aretha.

"Mimi nadhani ziko sawa na zinahitaji kuzinduliwa na kufanyiwa mnada ikibidi"

Walikuwa nje sasa, Aretha akashtuka na kugeuka kumwangalia Ed, "unadhani zitanunuliwa?" Akauliza Aretha kwa matarajio makubwa

"Sio tu kununuliwa Retha, zitanunuliwa kwa bei nzuri kuliko unavyowaza" Ed akamjibu

"Nitajaribu, kuna mkufunzi mmoja aliomba nimpe moja ya picha nilichora kwenye kuandaa mradi wangu darasani, yangu kumpa hajarudisha majibu yoyote anasema niendelee kuchora."

"Kweli hajajua uchoraji japo anawafundisha" Ed akajibu wakati akiweka vyema ile picha kwenye kiti cha nyuma japokuwa hakuwa ameitia machoni

"Retha" akaita wakati kasimama pembeni akijiandaa kuingia garini kwa safari ya kurudi.

Aretha aliyesimama hatua chache kutoka yeye aliposimama akaitika "Abee"

"Nakuahidi hii kazi itaenda hewani hivi karibuni. Nimeona picha mbili tu nimevutiwa, naamini wengine watavutiwa zaidi."

Aretha akainama chini na kumshukuru japokuwa hakuwa na uhakika kama yeye binafsi yuko tayari.