MTUNZI HALISI.
(2021)
Na. Batholomew Michael.
Riwaya.
____________________________________________________
Akiwa na miaka ishirini na tano, kijana SAUTI MAKINI ,Mtunzi chipukizi wa filamu asiye na mafanikio na mwenye mahangaiko makubwa kiuchumi, anatumika kama mtunzi wa siri (Ghostwriter) wa filamu ya kimapinduzi iitwayo MOTO NDANI YANGU na kumsababishia matatizo makubwa mwandaaji,muigizaji na anayedhaniwa kuwa mtunzi wa filamu hiyo TOMMY ABLOH. Baada ya kufichua siri nzito za uhalifu uliofanywa na familia maarufu ya mwanasiasa SALMAN KIDOLE kupitia filamu hiyo, hatimaye SAUTI anakubali kujitokeza kukabili matokeo ya utunzi wake akiwa kama MTUNZI HALISI wa simulizi ile ambaye alilaghaiwa, kisha jina lake kufichwa na sifa ya utunzi ule ikabaki kwa muandaaji TOMMY ABLOH.
Je, nini kitampata SAUTI Baada ya kujitokeza?
MTUNZI HALISI ni simulizi ya Matumaini, uwajibikaji na Ukombozi iliyojihusisha zaidi na mazingira ya Tanzania.
Kwa,
Wanangu Tyson na Batholomew Jr,
Ili waweze kusikiliza sauti za ndani ya mioyo yao.
Ikiwa unachowaza, unachoongea na unachofanya vinafanana, Wewe ni Mashuhuri.
____________________________________________
Kitabu hichi ni cha simulizi ya kubuni.
Hakuna muhusika aliyechorwa kutoka katika maisha ya mtu halisi au matukio halisi yaliyotokea.
Kama Kuna tukio lolote au muhusika aliyefanana na mtu halisi katika kitabu hichi haikudhamiriwa.
SURA YA 01: NDOTO MBAYA.
_______________________________________________
Ni usiku wa saa mbili,nilikua sebuleni nimekaa chumba cha kulia chakula, laptop yangu ipo mezani nikiendelea kuandika script ya filamu ambayo nilikua nina matumaini makubwa siku moja itakua mbele ya macho watu katika runinga na itachezwa na waigizaji wakubwa nchini, ingawa sikujua hayo yote yangetokea vipi ikiwa mpaka muda ule hakuna niliemjua wakunisaidia kupata nafasi ya kuwasilisha script zangu za filamu kwa waandaaji.Anafika Tamari,mdogo wangu pekee wa kike wa miaka 16 anawasha runinga anabadilisha vituo ili apate palipo na muziki au filamu kwani ndicho kilevi chake kikubwa sawa na wasichana wengi wa umri wake,na huwa anazozana na Mama mara nyingi tu kutaka kuangalia muziki kila muda na kujisahau kusoma,hata muda Mama akitaka kutizama vipindi anavyopenda, alibadili na kufika kwenye kituo kilichotangaza habari kuhusu uchunguzi unaoendelea wa tukio la kuungua kwa kiwanda cha sabuni cha SO CLEAN DETERGENT COMPANY wiki mbili zilizopita na kusababisha vifo vya watu zaidi ya ishirini na tano, na mimi nikiwa ni mmoja wa vibarua walionusurika katika Moto huo; kwakua siku hiyo tulipangiwa kazi ya kupakia mifuko ya sabuni katika magari.Tamari anasema "mmh Kaka wanaonesha kiwanda chenu kilivoungua" ,nikamjibu huku siangalii "aah toa tu, wahuni tu hao, uchunguzi hautorudisha ajira zetu wala maisha yaliyopotea", anaweka kituo kingine Mimi naendelea kuandika katika laptop yangu ananiita "Kaka ona Halle Morgan na Tommy eti wamegawana kampuni yao baada ya kupeana talaka", nilishtuka na kuinuka kusogea kwenye runinga, "hee! jamani hawa ndo walikua wanaleta mapinduzi kwenye filamu sijui wameshindana nini masikini, SPEEDOM PICTURES ndo inakufa hivyo asee", Tamari anajibu "Jamani mi Halle nampenda sijui kwanini kamuacha Tommy?",nikamjibu "Hao watu maarufu Wana mambo mengi huwezi kujua", katika habari wakasema inawezekana Tommy atarudi Nigeria alipokulia kwani Baba yake ni Mnaijeri na Mama yake ni Mtanzania. Habari ilinishtua na nikapata mfadhaiko kidogo kwani hawa ndiyo watu walionivutia kuanza kuandika script nchini kwetu licha ya kuwa mfatiliaji wa filamu za nje ila nchini hawa ndiyo walikua role models wangu na nilikua na ndoto za kufanya nao kazi.
Usiku nilipolala taswira za wenzangu walivyoungua Moto kiwandani mpaka kufa zilizidi kunirudia na kunitesa njozini, niliposhtuka saa 9 usiku niliwasha taa na kuwasha laptop yangu Kisha kujaribu kuandika Script niliyokwisha kuianza kuandika ya filamu niliyoiita "MOTO NDANI YANGU" iliyohusu ajali ile ya Moto na ushuhuda nilionao kuhusu chanzo Cha ajali ile, ndoto hizi zilikua zinafululiza kwani sikuwahi kushuhudia mtu akipoteza maisha hususani kwa maumivu kama kuungua na Moto.
Nilijikuta naandika script hii kwa kasi sana ingawa ilitokea mara kadhaa kushindwa kuandika kutokana na kushikwa na hisia na kujikuta nalia hasa nikifikiria rafiki zangu waliopoteza maisha kiwandani na familia zao zilizobaki hazina tumaini lolote baada ya kuwapoteza Bread winners au wasakatonge wao.
Jua lilipoanza kuangaza niliamka nikafagia uwanja kwakua ajira kiwandani haikuwepo tena, nikamuona Mama anatoka ndani akasimama mlangoni, "we SAUTI mbona mapema Baba na kufagia uwanja si umuamshe mdogo wako afagie?", nikamtizama nikatabasamu "Mama namsaidia tu, alafu leo umechelewa kibandani au?", Mama akaguna na kusema kwa kusikitika "amna Baba mtaji umekata,hapa kichwa kinaniuma acha tu", nikaacha kufagia na kumsogelea ili tusiongee sauti kubwa zaidi "Mama mbona hukuniambia?",.