"Waziri,nimeongea na vijana tayari,nahisi kazi muda si mrefu itafanyika",sauti ilisikika.Huyo alikuwa ni mtu wa karibu kabisa wa waziri huyo."Nachokitaka ni kwamba tunamng'oa moja kwa moja waziri mkuu kwa iyo mpango wenu uwe imara kweli kwelikweli." Waziri aliteta. "Bila shaka mkuu, Inshallah yatatumia." James alikuwa ni mtu wa karibu sana wa waziri kiasi kwamba alijua siri nyingi za waziri huyo.
"Vijana kazi inafanyika kesho Ijumaa saa sita na nusu mchana,be ready,kama kawaida atakayevurunda muwahishe kuzimu akatuandalie makao." Sauti ya James ilisikika.
⭐⭐⭐⭐⭐⭐⭐⭐⭐⭐⭐
" Oya Benson eeh , mbona mawazo kama yote kwani vipi, au bado Ana anakusumbua ?", Dominic alihoji. Dominic alikuwa ni rafiki wa karibu sana wa Benson kiasi kwamba waliweza kuelezeana shida zao ili kuzitatua kwa pamoja. Kiuhalisia Dominic alikuwa tajiri na haikueleweka chanzo cha utajiri wake. Hilo jambo lilikuwa ni kitendawili kwa Benson kwani hakuweza kuelewa chanzo hasa cha utajiri mkubwa wa Dominic. " Dah, sina kazi ,bado nimerudi kuishi kwa mshua, Ana kaniacha, yaani niponipo tu." , Benson alilalama. Dominic alimsikiliza kwa makini na akawa amepata suluhisho kwa matatizo ya Benson. "Benson naweza kukutafutia kazi ila je utaweza ?" ,alihoji Dominic ambaye alikuwa ni mtu aliyejengeka kimwili kuashiria kwamba ni mtu wa mazoezi mazito. " Oya mwamba eeh mi kazi yoyote ile napiga ilimradi nipate utajiri kama wako."
Dominic alisita kuongea ila akili yake ilimtuma kwamba Benson ataweza hii kazi. "Nisikie sasa mwanangu sana, hii kazi ni ya udereva na niamini mimi utapata chafu na naomba usiniulize maswali subiri ujionee" Dominic aliteta. Benson alipigwa na butwaa karibia dakika mbili zilipita na hakuelewa mantiki ya hii ajira atakayoenda kupewa. Mawazo yalimjia lukuki kichwani mwake na moja la wazo alilolipata ni kwamba asifanye hiyo kazi lakini alivyotafakari kwa upande mwingine akakumbuka sentensi ya mwisho ya Dominic kwamba atajionea mwenyewe. Hiyo sentensi ilimpa chachu ya kutaka kufanya hiyo kazi ya udereva.
" ila kama mimi nakuwa dereva we unafanya kazi gani?"Benson hakuacha kuuliza maswali yani kama vile hakuwa na shida kwa vile Dominic ni mshkaji alimchukulia poa tu. "Ok, mimi nafanya kazi chini ya jamaa mmoja anaitwa James. Huyo James anafanya kazi chini ya waziri mkubwa tu hapa nchini", aliendelea "na kuhusu mimi kufanya kazi gani utajua tu hivi karibuni ila hii kazi tunafanya very professional, sijui unaelewa ?".Kwa vile Benson alikuwa katika matatizo makubwa ya kiuchumi hakuweza kusema hapana. Pale alipotajiwa hela tu ni kama aliwàshiwa taa kwenye kiza. Aliikubali kazi.
Dominic akampigia James kumweleza kuhusu ingizo jipya.
" Ingizo jipya bosi."
" Safi mlete saa sita"
"Afu kingine bosi...
Simu ilikuwa imeshakatwa muda mrefu tu na James. Dominic alibaki akitafakari tu muda wote kabla ya kunena chochote. " Oya baadae mida flani ya wanga tunapotea tunaenda kumuona bosi", Dominic alianza kuongea toka akatiwe simu. " Kwa hiyo kuonana na huyo bosi ni lazima saa sita ya usiku ? Kwani hatuwezi kuonana naye mchana?" ,Benson alihoji. " Oya babu hizi kazi hazihitaji maswali we tulia tu ujionee". Dominic alifura hasira sasa kutokana na maswali ya kipuuzi ya Benson. Benson alishuhudia hizi kauli kwenye filamu tu ila hakuwahi kuzisikia mubashara hususan ikitoka kwa rafikiye.
🎵🎵🎵🎵🎵🎵🎵🎵🎵🎵🎵🎵🎵🎵
🎼'Humu ndani kuna mamilooo' 🎼
🎼'Nani kamuona huyo '🎼
🎼'Anacheza dansi gani uyo(oooh)'🎼
🎼'Yani ananesa soko,,🎼
🎼'Mi nabaki kujiramba dooo🎼
🎼'shikamoo dada nipe kidogo🎼
Yalikuwa ni mashairi ya wimbo pendwa wa msanii Rico Brizzo nchini. Usiku huo alikuwa akiperform katika uwanja wa Benjamin Mkapa na watu walijaa kwelikweli. Rico Brizzo alikuwa ni msanii aliyejua kupiga shoo nzuri ya mziki kiasi kwamba aliwakonga nyoyo mashabiki zake na hilo lilipelekea kufananishwa na wasanii wakubwa duniani kama Prince. "Oya Rico , waandishi wa habari wanakusubiria hapo nje ufanye nao mahojiano." Hiyo ilikuwa ni sauti ya meneja wa Rico Brizzo aitwaye Dano. Ilikuwa ni muda mchache toka atoke kupiga shoo.
" Vipi shoo ya leo Rico naona mashabiki wana furaha"
" Rico, Safari hii unaachia album au Ep "
" Eti tunasikia umeachana na Lily na sasa hivi una toka na pisikali nyingine ya kishua. Na kingine umeachana na Lily kwa sababu gani."
Yalikuwa ni maswali mfululizo alioulizwa na waandishi, Rico hakuelewa ajibu lipi aache lipi ila akaamua ajibu swali la tatu mana lilimkaa kichwani. " Ni kweli nimeachana na Lily. Ila sina majibu kwa maswali mengine. Nimechoka sana naomba mnipishe niende kupumzika." "Ila tunasikia huyo demu uliokuwa nae umemnyang'anya mtu", paparazzi mmoja alisikika.
Rico alifura hasira kiasi kwamba aliondoka hapo bila kujibu chochote. Lilikuwa ni swali ambalo hakulitarajia. Akaelekea moja kwa moja kwenye gari yake aina ya Toyota Rumion. "Wapi tunaenda,bosi" alihoji dereva. Mahmoud alikuwa ni dereva wa muda mrefu wa Rico Brizzo kiasi kwamba alijua siri nyingi za msanii huyo. "Twende kwenye nyumba yangu ya Kawe", alijibu Rico. Njiani Rico hakuacha kuliwaza swali la mwisho aliloulizwa na waandishi wa habari. ' Yaani Ana alikuwa ni mpenzi wa mtu. Mbona hajaniambia na wale mapaparazi wamejuaje ? ', Yalikuwa ni mawazo ya Rico aliyoshindwa kuyapatia ufumbuzi. " Bosi tumefika"
Rico Brizzo alishuka kwenye gari na kuelekea moja kwa moja nyumbani kwake. Hakuweza kutulia kwa namna mawazo yalivyoshambulia kichwa chake akaamua ampigie simu Ana kumtaka aje nyumbani kwake. Baada ya Ana kupigiwa simu aliondoka nyumbani kwao takriban mida ya saa sita na nusu usiku na kuelekea kwa Rico. Ana hakujizatiti katika penzi la Rico ila alitaka umaarufu tu na alikuwa tayari kufanya lolote kumridhisha Rico ilimradi apate umaarufu. "Hodi! hodi baby beiii...bi" . Ana alitoa sauti ya deko la kimahaba. " Ingia". Sauti ya Rico haikuonyesha kama kuna usalama kwa Ana. Ana akaingia chumbani humo na kuketi kitandani.
" Babe mbona umekunja sura hivyo vipi kwani?" Ana alihoji. "Yaani sikiliza mimi naachana na wengi sana kwa sababu hawaijui mapenzi na nikakuona wewe ni mtu wa maana kumbe na wewe jau tu." " yaani kumbe una dume lako halafu unanichora tu. Nakuuliza umefuata nini kwangu? Nakuuliza tena umefuata nini kwa.....(iiiiihiiii)" Rico alianza kulia kama mtoto aliyepigwa bakora kwa kuonewa. Alikuwa na michubuko kwenye moyo. Wanawake wengi waliuvunja moyo wake vipande vipande. Alikuwa anatafuta mpenzi wa kuponya majereha yake ya moyo. Alianza kuvunjwa moyo katika mapenzi toka alivyokuwa sekondari huko. Lakini moja ya jambo lililomuumiza sana licha ya ustaa wake, mpenzi wake wa zamani aitwaye Judy alipomsaliti na kutembea na bodyguard wa Rico. Jambo hilo lilimuumiza sana Rico kiasi kwamba akaachana na biashara ya kulindwa na mabodyguard. Rico alipata umaarufu,pesa na wanawake ila alikosa upendo wa kweli.
"Honey, nisikilize basi huyo unaemsikia kwamba ni mpenzi wangu ni uongo bali alikuwa rafiki yangu tu zamani na kingine yeye anatoka na yule rafiki yangu aitwae Rose, si unamjua Rose babe ?" ,Ana aliongopa. " Kweli baby unachosema?" , alihoji Rico." Yes, babe kwanini nikuongopee tena leo nataka nikupe sukari ujilambe hadi ung'ate vidole vyako.We si umetoka kupiga shoo sasa hapa nakupa shoo yangu mimi hautaamini." Ana alichombeza. Rico hakuchelewesha alianza romanza za kufa mtu na alipompatia Ana mhogo wa Jang'ombe aung'ate ubao ulisomeka... Ni asubuhi sasa.